Idara ya Kilimo, Umwagiliaji na Ushirika ni moja ya idara zilizoko katika Halmashauri ya Mji wa Geita kutokana na ukweli kwamba asilimia 77 ya wakazi wa Halmashauri ya Mji wanajishughulisha na Kilimo, na kwamba kilimo kinachangia asilimia 73 ya pato la Halmshauri.
Halmashauri ya Mji Geita ina jumla ya hekta 51,600 zinazofaa kwa kilimo lakini mpaka sasa eneo linalolimwa ni hekta 21,200 tu. Halmshauri ya Mji Geita inayo mabonde yenye jumla ya hekta 1,560 kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji kwa mazao ya mpunga,mbogamboga na matunda.
Tunazo fursa nyingi za kutekeleza kilimo ikiwemo uwepo wa vyanzo vya maji kwa ajili ya upatikanaji wa maji,ardhi yenye rutuba,wataalam, masoko ya bidhaa mbalimbali za kilimo na uongozi imara ambao wanatoa mchango mkubwa katika sekta ya kilimo ikiwemo kutafuta wafadhili watakaowasaidia wakulima kuzalisha zaidi na kuongeza kipato chao.
Zipo changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya kilimo katika Halmashauri ya Mji. Mojawapo ni wakulima kutegemea mvua, bei kubwa za pembejeo na upungufu wa zana za kisasa, uhaba wa masoko, na uvamizi wa visumbufu vya mazao. Ili kutatua changamoto hizi, ni vema Serikali katika ngazi zote ikatilia mkazo katika uanzishaji wa skimu za umwagiliaji katika mabonde tuliyonayo kwani hali ya mabadiliko ya tabia nchi inaendelea kuwa chagamoto kubwa kwa wakulima na pia kutoa ruzuku kwenye bei za pembejeo.
Pia wakulima wasaidiwe kupitia vikundi vyao wenyewe, taasisi za kifedha na wafadhili mbalimbali kupata pembejeo na zana za kisasa ili waweze kuzalisha zaidi.
SHUGHULI ZINAZOTEKELEZWA:
Kutoa mafunzo ya kanuni bora za kilimo kwa wakulima ikiwemo upandaji kwa nafasi na kwa wakati, matumizi ya pembejeo, zana na teknolojia za kisasa, teknolojia za umwagiliaji na kilimo hai. Mafunzo haya yanatolewa kwa njia mbalimbali ikiwemo mihadhara, mijadala, mashamba darasa na mashamba ya mfano.
Kutoa mafunzo ya matumizi bora ya ardhi kwenye maeneo ya kilimo kwa kupanga na kugawa matumizi ya ardhi kwa shughuli mbalimbali ikiwemo kuongeza uzalishaji kwa eneo.
Kutoa taarifa mbalimbali zinazohusu sekta ya kilimo, mfano ni wapi pembejeo zinapatikana, hali ya masoko, uwezesho wa kifedha na hata mashirika yanayowasaidia wakulima kupata mahitaji yao mbalimbali
Kuwasaidia wakulima kuanzisha na kutunza vitalu vya mbegu za mboga na matunda kwa ajili ya kukuza mazao ya bustani
Kufanya maonesho mbalimbali kupitia siku za wakulima, na hata ngazi ya wilaya kupitia maonesho ya nanenane.
Kutoa mafunzo ya hifadhi ya mazao ya kilimo kwa kuzingatia viwango vinavyohitajika na matumizi ya viuatilifu vya mazao ya kilimo ghalani.
Kuwatembelea wakulima, kuona changamoto wanazokutana nazo na kutoa ushauri wa jinsi ya kutatua changamoto hizo.
Kutoa tuzo na zawadi mbalimbali kwa wakulima ili kuwahamasisha wenzao kupenda kufanya vizuri zaidi. Hii inaleta ushindani ambao hatimae unasababisha ongezeko la uzalishaji kwa ujumla
JINSI HUDUMA ZINAVYOPATIKANA
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa