Leo, 3 Desemba 2025 – Halmashauri ya Manispaa ya Geita imefanya zoezi la kukabidhi kompyuta mpakato (laptop) tano kwa Maafisa Maendeleo ya Jamii wa kata, ikiwa ni hatua ya kuongeza ufanisi wa utendaji kazi kwa kutumia teknolojia.
Zoezi hilo limefanyika katika ukumbi wa Manispaa hiyo, likiongozwa na Mkurugenzi wa Manispaa, Ndugu Yefred Myenzi.
Akitoa taarifa hiyo Ndugu Robert J. Sungura Mkuu wa Divisheni ya Maendeleo ya Jamii, amesema kuwa idara imeona umuhimu wa kugawa vifaa hivyo ili kuwawezesha watumishi kwenda sambamba na kasi ya maendeleo ya teknolojia, jambo litakalosaidia kuboresha utoaji huduma kwa jamii.
Amezitaja kata zilizonufaika katika awamu hii ya kwanza kuwa ni Kalangalala, Nyankumbu, Buhalahala, Shiloleli na Ihanamilo, huku akibainisha kuwa mpango uliopo ni kufanikisha upatikanaji wa vifaa kwa kata nyingine zilizobaki.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Myenzi ameipongeza Divisheni ya Maendeleo ya Jamii kwa namna inavyotekeleza majukumu yake kwa ushirikiano na viongozi wa ngazi zote. Ameeleza kuwa kompyuta hizo zitaongeza usiri wa taarifa, kupunguza matumizi yasiyo rasmi ya steshenari, na kuongeza ubora wa kazi.
“Vifaa hivi vitumike kwa malengo yaliyokusudiwa, hasa katika kuchakata taarifa za waombaji mikopo na shughuli nyingine za kiofisi. Hii ni mali ya Serikali, hivyo tunatarajia itatunzwa kwa uadilifu ili viweze kutumika na wengine watakao kuja,” amesema Mkurugenzi Myenzi.
Amesisitiza kuwa hatua hii ni sehemu ya kuimarisha mifumo ya utendaji kazi kwa Maafisa wa ngazi ya kata, sambamba na kupunguza muda wa utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa