Mkuu wa Mkoa wa Geita Mh. Mhandisi Robert Gabriel amewaagiza Waheshimiwa Madiwani wa Halmashauri ya Mji Geita kuchagua miradi ambayo itapewa kipaumbele na wananchi husika kwa lengo la kuanzishwa au kuendelezwa, na kuhakikisha wanaisimamia vyema miradi hiyo ili iwe endelevu.
Mkuu wa Mkoa ametoa kauli hiyo wakati wa Mkutano wa Baraza la Madiwani hivi karibuni, baada ya kuonekana kwa mfumo uliokuwa umezoeleka wa Kampuni ya Dhahabu ya Geita kuchagua miradi ambayo wanaitekeleza katika jamii kupitia mchango wao kwa jamii inayowazunguka, pasipo ushirikishwaji wa awali wa kuchagua kwa pamoja miradi ya maendeleo pamoja na wananchi waishio katika maeneo ya utekelezaji mradi.
“Miradi inayopangwa kutekelezwa na GGM inatakiwa ipendekezwe na watumiaji ambao ni jamii inayotambua vipaumbele vyake. Wananchi wana matumaini makubwa na Madiwani kwa sababu nyie ndio wawakilishi wao na mna majibu sahihi kwa wananchi waliowachagua ili kuwasaidia katika utatuzi wa changamoto zinazowakabili”. Aliongeza Mhandisi Robert Gabriel.
Mkuu wa Mkoa wa Geita pia amewatahadharisha watumishi wa Umma na watu wote wanaohusishwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kutovuruga, kuchezea fedha au kuyumbisha uchumi wa Mkoa wa Geita kwa namna yeyote. Mtu wa namna hiyo hatavumiliwa bali atachukuliwa hatua madhubuti za kisheria.
Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Geita amewasihi watumishi wa Umma wasio waaminifu ambao hutumia fedha za miradi kujinufaisha wao binafsi kuacha tabia hiyo, kwa sababu watu hao wamekuwa wakikwamisha maendeleo ya Mkoa na wanatakiwa kushughulikiwa ili kuwa na miradi yenye ufanisi.
Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Mhandisi Robert Gabriel amewataka Waheshimiwa Madiwani wa Halmashauri ya Mji kuchagua Miradi inayohitajika kwa wananchi wao na kuisimamia kikamilifu
Mbunge wa Geita Mjini Mhe. Costantine Kanyasu akieleza namna wananchi wa Geita wanavyotakiwa kutunza na kulinda miradi inayoanzishwa na Serikali katika maeneo yao.
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa